ACT Wazalendo Wakataa Wito wa Polisi
Novemba 2, 2017, Chama cha ACT Wazalendo kilipokea wito toka kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI) wa kuwataka Wajumbe wote wa Kamati Kuu ya ACT Wazalendo wafike Kituo cha Makosa ya Fedha (Financial Crime Unit) kilichopo Maeneo ya Kamata, Kariakoo Jijini Dar es salaaam kwa ajili ya mahojiano siku ya Jumatatu, Novemba 6, 2017.
Ikumbukwe kuwa wito huu unakuja baada ya Kiongozi wa Chama, ndugu Kabwe Z. Ruyagwa Zitto kuhojiwa katika kituo hicho kwa takribani masaa matatu Oktoba 31, 2017 kutokana na Taarifa ya Chama kuhusu Kusinyaa kwa Uchumi.
Uamuzi huu wa kuihoji Kamati Kuu nzima unashangaza sana kwa sababu mbili:
i. Kamati Kuu ni chombo cha kitaifa cha Chama chenye mamlaka ya kufanya maamuzi kwa mujibu wa katiba ya ACT Wazalendo kama chombo na si kama mjumbe mmoja mmoja.
ii. Jeshi la Polisi halina madaraka ya kushughulikia wala kuingilia maamuzi halali ya vyombo (organs) katika vyama vya siasa.
Tangu tuzindue kampeni zetu katika kata ya Kijichi, Jeshi la Polisi limefanya maamuzi ya kushikilia au kuhitaji kuwahoji viongozi wetu, maamuzi ambayo kwa namna moja au nyingine yanaathiri kampeni zetu. Kwa maamuzi haya ya Jeshi la Polisi, ni wiki sasa inakatika viongozi wetu wakilazimika kusalia jijini Dar es salaam kusubiri kuhojiwa na Polisi.
Uamuzi wetu ni kuwa tutaendelea na kampeni kama kawaida. Polisi watafute namna na wakati sahihi wa kufanya mahojiano na viongozi wetu. Tunawaomba viongozi, wanachama wa ACT Wazalendo na wananchi kwa ujumla kuendelea na kampeni za udiwani wakisisitiza ujumbe wetu wa UCHUMI na HAKI.
Yeremia Kulwa Maganja,
Kaimu Mwenyekiti wa Chama – ACT Wazalendo.
Novemba 5, 2017
Dar es salaam
>
No comments: