Katibu Mkuu Chadema Wilaya ya Simanjiro ajiengua na Kuhamia CCM

Katibu wa Chadema Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Meshack Tureto amejiengua ndani ya chama hicho na kujiunga na CCM.

Tureto aliyekuwa pia katibu wa mbunge wa Simanjiro, James ole Millya ametangaza uamuzi huo akidai Chadema imepoteza dira na mwelekeo wa uongozi.

Anakuwa kiongozi wa pili wa Chadema wilayani Simanjiro kujiuzulu baada ya Jumamosi Novemba 25,2017 katibu wa uenezi, Ambrose Ndege kujiuzulu wadhifa huo na kujiunga na CCM.

Ndege alikabidhi kadi ya Chadema kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.

Tureto amesema amefikia uamuzi baada ya kuona viongozi wenzake hawana mikakati wala mipango ya maendeleo.

Tureto amesema awali, alikuwa mtendaji wa Kijiji cha Narakauwo kilichopo Kata ya Loiborsiret kwa tiketi ya CCM lakini aliacha na kufuata mabadiliko Chadema.

Amesema chini ya uongozi wa Rais John Magufuli, mambo yanakwenda kama alivyotarajia hivyo hana sababu ya kuendelea kuwa Chadema.

"Chadema imepoteza mwelekeo sasa, nimeona nirudi CCM ambako hakuna kujilimbikizia vyeo na kila mwanachama ana haki kwa kuwa hii ni CCM mpya," amesema Tureto.

Amesema hakuingia Chadema kwa lengo la kupata masilahi bali alijiunga kwa utashi wake kama ambavyo sasa ameondoka na kurudi CCM.

Mbunge wa Simanjiro, James ole Millya amemtakia Tureto heri anakokwenda. Amesema sababu alizotaja za kuondoka Chadema hazina mashiko.

Ole Millya amesema Tureto aliingia Chadema kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 baada ya kuona yeye ana nafasi kubwa ya kuwa mbunge wa Simanjiro.

Amesema Tureto alikuwa mtendaji wa Kijiji cha Narakauwo na alifukuzwa hivyo aliomba apatiwe nafasi naye akamjibu hana sifa.

Ole Millya amesema Tureto hakuwa katibu wa Chadema aliposhinda ubunge mwaka 2015 bali Frank Oleleshwa ambaye miezi sita iliyopita alipojiuzulu ndipo naye akashika nafasi hiyo.

"Wengi wanatafuta mafanikio binafsi na utajiri, lakini ukweli utabaki palepale CCM haitatawala milele Tanzania," amesema Ole Millya.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Jackson Sipitieck amempongeza Tureto kwa kujiunga na chama hicho na amemhakikishia ushirikiano wa kutosha.
>

No comments: