SAA 120 ZA LULU GEREZANI,UCHUNGUZI WA NPASHE WABAINI MAZITO,MIJADALA KILA KONA

WAKATI leo ikiwa ni siku tano zimepita tangu Elizabeth Michael (Lulu) aende gerezani kutumikia kifungo cha miaka miwili, baada ya kukutwa na hatia katika kesi ya kumuua bila kukusudia mpenziwe Steven Kanumba,- Msanii huyo wa filamu na mitindo ameendelea kuwa gumzo katika maeneo mbalimbali ikiwamo kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii. Lulu alihukumiwa kwenda kutumikia kifungo siku ya Novemba 13, hivyo kupita siku tano hadi kufikia leo, sawa na saa 120 (siku moja ina saa 24).

            Alikutwa na hatia ya kuua bila kukusudia kutokana na kifo cha Kanumba kilichotokea mwaka 2012. Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa tangu Lulu aende gerezani Jumatatu iliyopita, picha zake mbalimbali zimeendelea kurushwa kwenye mitandao ya kijamii, huku baadhi ya watu wakiibua mijadala inayohusiana na kutoendelea kuonekana uraiani katika kipindi chake cha kutumikia kifungo. “Ukifuatilia mijadala inayoendelea mitaani na kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, utagundua kuwa Lulu ana mvuto wa aina yake…licha ya kuwa gerezani kwa siku hizi kuanzia Jumatatu, lakini bado ameendelea kuwa gumzo na inaelekea hali hii itadumu hadi siku atakayokuwa huru,” mmoja wa wafuatiliaji wa filamu za nyumbani maarufu ‘bongomovie’ aliiambia Nipashe jana kuhusiana na Lulu.

Aidha, akizungumza na Nipashe jana, msanii wa filamu aliyewahi kufanya kazi mbalimbali na Lulu na pia Kanumba, Yvonne Cherly (Monalisa), alisema kuzungumzwa kwa Lulu na mijadala mbalimbali kuhusu yeye inayoendelea kwenye mitandao ya kijamii ni dalili kwamba yeye ni kipenzi cha watu. Hata hivyo, Monalisa alisema kuwa hilo siyo jambo la ajabu kwa sababu mwisho wa siku, mijadala hiyo itakoma na maisha yataendelea kama kawaida. “Naamini watazungumza mwisho watachoka na kuacha wenyewe… na mimi siko upande wowote wa Lulu wala Kanumba kwa sababu wote walikuwa ni rafiki zangu,” alisema Monalisa. Akieleza zaidi, Monalisa alisema kuwa anawaonea huruma wote kwa sababu Lulu bado ni kijana mdogo na pia Kanumba alifariki akiwa kijana mwenye ndoto nyingi za kimaisha.

Mimi nawaonea huruma wote kwa sababu ni vijana na pande zote za familia zimeathirika. Walikuwa na majukumu ya kufanya, lakini mmoja kapoteza maisha na mwingine yupo na mahakama imeshafanya kazi yake,” alisema. Kadhalika, baada ya hukumu ya Lulu, msanii wa muziki wa kizazi kipya, Afande Sele, alikaririwa akitoa maoni ya kumuonea huruma Lulu na kudai kuwa wakati wa tukio hakustahili kuwa mpenzi wa mtu kutokana na umri wake. Baada ya ujumbe huo unaodaiwa kuwa wa Afande Sele kusambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, msanii mwingine wa filamu, Steve Nyerere, naye aliibuka na kutoa yake, akimkosoa Afande Sele. Msanii mwingine wa filamu, Mahsein Awadh maarufu kwa jina la Dk. Cheni, ambaye alikuwa karibu na Lulu wakati wote wa kesi yake iliyokuwa ikiendelea mahakamani kabla ya hukumu kutolewa, kupitia ukurasa wake wa Twitter, aliwasihi watu kuelewa kuwa matukio aina hiyo yanaweza kumkuta mtu yeyote.


Kikubwa tumuombee (Lulu), maneno maneno hayafai, pengine akiyasikia hatujui yatamuumiza kiasi gani… tumuombee kwa sababu bado ni mtoto mdogo,”aliandika Cheni. Aidha, katika saa hizo 120 za Lulu kuwa gerezani, mbali na wale wanaomfariji, wapo pia waliokuwa wakijadili kwa maoni ya kuonyesha kuwa ashukuru kwa adhabu aliyopata kutokana na sheria za nchi.

CHANZO NIPASHE
>

No comments: