SIMBA YAMTEKA ASANTE KWASI KWA SAA NNE

Beki wa kati wa Lipuli FC, Asante Kwasi raia wa Ghana (mwenye jezi namba 13) akifanya yake uwanjani.

BEKI wa kati wa Lipuli FC, Asante Kwasi raia wa Ghana, muda wowote anaweza kuwa mali ya Simba baada ya klabu hiyo kuanza mazungumzo ya chinichini na viongozi wa Lipuli pamoja na mchezaji mwenyewe.

Simba ambayo hivi sasa ina upungufu kwenye nafasi ya ulinzi, imeliweka jina la Kwasi kuwa chaguo la kwanza baada ya Mghana huyo kuwa na kiwango cha juu tangu msimu uliopita.

Mara baada ya mchezo kati ya Simba na Lipuli, taarifa zinasema kuwa viongozi wa Simba walitumia zaidi ya saa nne kuzungumza na mchezaji huyo kabla hajapanda ndege kwenda nchini kwao Ghana kwa matatizo ya kifamilia.
Kwasi huu ni msimu wake wa pili katika Ligi Kuu Bara ambapo msimu uliopita alikuwa akiitumikia Mbao FC ya Mwanza ambapo aliachana nayo mwishoni mwa msimu huu na kutimkia Lipuli.
“Tunamtaka Kwasi aje aongeze nguvu kwenye kikosi chetu ambacho
kinaonekana kuwa na upungufu kwenye nafasi ya ulinzi hasa beki wa kati. Hivi sasa Salim Mbonde ni majeruhi, Juuko Murshid anamaliza mkataba wake na inaonekana anaweza kuachwa.

“Method Mwanjale hana uwezo wa kucheza mara kwa mara kutokana na umri kuwa mkubwa, hivyo anahitajika mtu wa kuimarisha nafasi hiyo ambapo tumeanza mazungumzo na Lipuli juu ya kumalizana na Kwasi,” kilisema chanzo.

Championi lilifanya juhudi za kuwatafuta viongozi wa Lipuli kuzungumzia ishu hiyo, ambapo kocha wa timu hiyo, Selemani Matola alisema: “Taarifa hizo za beki wangu Asante Kwasi kutakiwa na Simba zipo lakini ni za chinichini, kama unavyojua yule ni beki wangu tegemeo katika ulinzi, hivyo itakuwa ngumu kumuachia.

“Lakini licha ya hivyo, kama Simba watakuja na dau zuri tutamuachia kisha hizo fedha tuzitumie kusajili wachezaji wawili au watatu. Dau ni siri, lakini ieleweke tu likiwa zuri tutamuachia tu kwa maslahi ya klabu, hakuna jinsi ingawa ni mchezaji bora sana kwetu.” Alipotafutwa Kwasi alisema: “Sina kipingamizi chochote kama meneja wangu akikubaliana nao kwani tunaangalia maslahi, kazi popote mimi nafanya wala sina shida na Simba.
Stori: Omary Mdose na Martha Mboma
>

No comments: