Tundu Lissu Asimulia Alivyonusurika Kupigwa Risasi ya Fuvu la Kichwa
Kwa mara ya kwanza, Tundu Lissu amezungumzia shambulio la kinyama alilofanyiwa na watu wasiojulikana kwa kueleza kuwa, alinusurika kufumuliwa fuvu la kichwa kwa risasi.
Lissu, Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), aliyasema hayo jana, jijini Nairobi anakotibiwa wakati akihojiwa na Jarida la Financial Times la Uingereza.
Yakiwa ni mahojiano yake ya kwanza tangu aliposhambuliwa nje ya makazi yake yaliyoko Area D, mjini Dodoma Septemba mwaka huu, Lissu mmoja wa wakosoaji wakubwa wa serikali alisema anaamini alikuwa mlengwa wa jaribio la mauaji.
Akizungumzia shambulio hilo dhidi yake, alisema sekunde chache baada ya watu wawili wenye silaha kushuka katika gari lililokuwa likimfuatilia kwa wiki tatu, derava wake alimsukuma chini ya sakafu ya gari lake wakati wakihangaika kukwepa risasi nyingi zilizoelekezwa kwenye gari lake, nyingi zilimpiga mgongoni na nyingine kwenye bega lakini risasi moja ilikosakosa kufumua fuvu lake la kichwa.
“Hali ikawa mbaya sana kwa sababu sikuweza kuhesabu risasi, naambiwa kwamba risasi 38 zilipiga gari langu na 16 zilinipata na moja iliyokuwa imelengwa kunifumua fuvu la kichwa ilinipiga begeni karibu na shingo,” alikaririwa Lissu.
Mwanasiasa huyo ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki na Mnadhimu wa kambi ya upinzani alikakririwa akieleza zaidi kuwa kilichotokea ni ushahidi wa kile ambacho amekuwa akikizungumzia mara nyingi kuhusu uwepo wa watu waovu wanaotekeleza kampeni ovu ya kuipeleka nchi pabaya.
Wakati Lissu akikutwa na mkasa huo mbaya, historia yake ya kisiasa inaonyesha kuwa amekwishtakiwa mara sita, mwaka huu kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya uchochezi.
Wachambuzi na wafuatiliaji wa mambo wamekuwa wakieleza kuwa shambulio hilo linaweza kuwa moja ya mikakati ya magenge ya wapinzani wa serikali waliobanwa na dola ambao sasa wanajaribu kutumia kila aina ya mbinu kuifarakanisha jamii hususan wanasiasa.
Tayari Jeshi la Polisi limekwishaanzisha uchunguzi wa tukio hilo na Inspekta Jenerali (IGP), Simon Sirro amekwitoa wito kwa mtu yeyote mwenye taarifa zinazoweza kusaidia uchunguzi huo kuzitoa kwa makachero wa polisi.
Sambamba na hilo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas naye alikutana na waandishi wa habari kuzungumzia tukio hilo ambapo alitoa rai kuwa shambulio hilo lisichukuliwe kisiasa kwa sababu ni uhalifu wenye sura za ile ile ya matukio ya kihalifu ambayo yamekuwa yakitokea nchini.
Katika mkutano wake na wanahabari alioufanya siku chache baada ya Lissu kushambuliwa, Dk. Abbas alionya kuhusu upotoshaji uliokuwa ukifanywa na baadhi ya watu waliokuwa wakijaribu kuipata matope serikali kwa kuihusisha na shambulio na aliwataka wote wenye taarifa zinazoweza kusaidia uchunguzi, akiwemo Lissu kutoa ushirikiano kwa polisi.
>
No comments: