YANGA SC YAKWEA PIPA KUFUATA STRAIKA UARABUNI
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga wamejitoa kwenye vita ya kumsajili mshambuliaji, Elias Maguli, huku bosi wake akikwea pipa kwenda Uarabuni kwa ajili ya kuvunja mkataba wa Danny Lyanga wa Fanja.
Maguli ni kati ya wachezaji waliokuwepo kwenye mipango ya kusajiliwa Yanga katika usajili huu wa dirisha dogo ambalo limefunguliwa Novemba 15, mwaka huu.
Lyanga aliwahi kuichezea Coastal Union ya Tanga kabla ya kutua Simba ambako hakudumu na kutimkia Urabuni.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, jina la Maguli limeondolewa na kamati ya usajili ya timu hiyo katika hatua za mwishoni za kutaka kumsajili.
Mtoa taarifa huyo alisema, kamati hiyo imeliondoa jina la Maguli kwa kigezo kuwa ni mzito na hana kasi ndani ya uwanja na baadaye kulipendekeza jina la Lyanga.
Aliongeza kuwa, kamati hiyo ilimfuatilia mshambuliaji huyo na kugundua ana mkataba wa mwaka mmoja na walivyomfuata kuzungumza naye yeye mwenyewe alikubali kuongozana na mabosi hao kwa ajili ya kwenda Uarabuni kuvunja mkataba na Fanja.
“Maguli alikuwa chaguo letu la kwanza kumsajili katika majina ya washambuliaji tuliyoyapendekeza wasajiliwe katika dirisha dogo, lakini baada ya kikao cha mwisho cha kamati tulipokea jina lingine kutoka kwa mwanakamati mwenzetu.
“Jina hilo ni la Lyanga na kikubwa alikuja na hoja ya msingi kuwa Maguli ni mzito na hana kasi, hivyo basi tumeiona hoja hiyo ya msingi lakini ukaja ugumu mwingine wa Lyanga kuwa bado ana mkataba na Fanja.
“Lakini tulipomfuata Lyanga mwenyewe alikubali kuwa anaweza kusaini na kuongozana na mabosi wa timu hiyo kwenda Uarabuni kwa ajili ya kuvunja mkataba Fanja kama ikiwa sawa basi atakuwa mali yetu lakini ikishindikana bado tutaendelea kupambana kwa kuwa bado tuna muda,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika kuzungumzia hilo alisema kuwa: “Sisi usajili wetu tunaufanya kimyakimya na tunatangaza baada ya kukamilisha kila kitu.
“Na usajili wetu tunaufanya kiufundi kwa kumshirikisha kocha wetu Lwandamina kwa kufuata mapendekezo yake aliyoyatoa katika timu, hivyo kila kitu kikikamilika ndiyo tunatangaza,” alisema Nyika.
>
No comments: