Askari wa 14 wa JWTZ wauawa katika shambulio nchini DR Congo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kuuawa kwa askari 14 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliopo katika operesheni ya ulinzi wa amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Pamoja na askari hao kuuawa, askari wengine 44 wamejeruhiwa na 2 hawajulikani walipo.
Kufuatia vifo hivyo Mhe. Dkt. Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Salvatory Mabeyo, Maafisa na Askari wa wote JWTZ, familia za marehemu na Watanzania wote kwa kuwapoteza mashujaa waliokuwa wakitekeleza wajibu wao.
“Nimeshtushwa na kusikitishwa sana na vifo vya vijana wetu, askari shupavu na mashujaa waliopoteza maisha wakiwa katika majukumu ya kulinda amani kwa majirani zetu DRC” amesema Mhe. Dkt. Magufuli.
Amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi, Amina.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania wote kuwa watulivu na kuwa na subira wakati Serikali ikiendelea kuchukua hatua zinazostahili baada ya kutokea tukio hilo, na pia amewaombea majeruhi wote wapone haraka ili waweze kuendelea na majukumu yao ya kawaida.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino, Dodoma
08 Desemba, 2017
>
No comments: