BONGO MUVI, PENDANENI MUWE BORA
NIMSHUKURU Mungu kwa kudra na rehema zake kwa sababu ya pumzi ya bure ambayo ninaitumia maishani mwangu.
Asante pia msomaji na mdau mkubwa wa Barua Nzito kwa maoni na ushauri wako kila mara. Maoni yenu ni mengi na mazuri sana, ninajitahidi kuyafanyia kazi kwa sababu wewe ndiye mshauri wangu mkubwa.
Leo ninapenda niwakumbushe wasanii wa Bongo Muvi ambao ninawakubali na wamefanya kazi nzuri na wanaendelea kufanya ila kuna mambo madogomadogo ambayo wanapaswa wayarekebishe ili kuikuza na kuitambulisha kazi yao nje ya mipaka ya Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Wiki iliyopita nilikuwa mmoja wa wadau wa filamu walioalikwa kwenye uzinduzi wa filamu ya msanii Issa Mussa ‘Cloud 112’ ya Usijisahau iliyozinduliwa kwenye Ukumbi wa Cinemax Century uliopo Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Nilienda kwenye uzinduzi ule kwa sababu ya kuangalia na kumuunga mkono Cloud kwa filamu yake ambayo kwa mara ya kwanza ameifanya akiwa nchini Sweden, waswahili wanasema kavuka boda tena nje ya Bara la Afrika.
Nikiwa kwenye zulia jekundu ambalo wasanii na wageni waalikwa wanapaswa kupita kwa ajili ya kupata pichapicha, nilishtuka sana kutokana na kuwaona wasanii wachache waliojitokeza kama kumuunga mkono akiwemo msanii Esha Buheti, Jacob Stephen ‘JB’ Daud Michael ‘Duma’ na wadau wengine akiwemo mgeni rasmi ambaye alikuwa ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye aliipongeza filamu ile kwa ubunifu na kuthubutu kwa Cloud.
Kwa filamu ambayo imefanywa na Mtanzania kwa kuwashirikisha Watanzania tena kwa kuwasafirisha nje ya nchi ni uthubutu mkubwa sana. Nilitegemea kuwaona wasanii kadha wa kadha wakiwa wamejazana katika kumuunga mkono mwenzao, lakini katika kuonesha kutowepo ushirikiano wa wasanii, hakika ilihuzunisha.
Nawashangaa sana wasanii wa Bongo Muvi ambao mmekuwa mkisema kuwa soko la filamu halijafa wakati hata kwenye kazi za wasanii wenzenu hamtokei.
Hata kama mna wivu, mna chuki, mlipaswa kuficha madhaifu hayo mbele ya mashabiki na wadau wengi wa filamu ambao walihudhuria kwenye uzinduzi huo.
Kwa taswira niliyoiona inaonesha kabisa wasanii wenyewe hamkubaliani, hampendani, hamuungani mikono, kwa maana nyingine hamuwezi kuikuza sanaa ya filamu kwa kudharauliana kwa kutokushirikiana. Huo ni unafiki, hiyo ni roho mbaya.
Kujitokeza kwenu wachache kwenye uzinduzi inaonesha ni kwa namna gani hampendani. Mbaya zaidi baadhi ya wasanii wanaoponda ‘ooh filamu haina jipya ni ya kawaida” acheni roho za mtimanyongo ndugu zangu.
Kama kweli nia yenu ni kurudisha soko na heshima ya kazi yenu basi ni lazima mshirikiane kwa pamoja. Ndiyo maana kila siku mnazidi kuzama kwenye tope zito, hamshituki tu kuwa mtadidimia kabisa, labda muongeze nguvu ya pamoja ili kujinasua na lenyewe mmeshindwa.
Ndugu zangu filamu za Kibongo zinazidi kupotea, amkeni, acheni umimi, acheni kuchaguana kwenye ‘sini’, acheni kuoneana wivu kama mtu kafanya vizuri mpe hongera yake kama kafanya vibaya mwambie au mpe ushauri siyo kuanza kumcheka chinichini, huo ni unafiki.
Ninaamini kabisa kwa vichwa vyenu kama mkiungana na kuondoa tofauti zenu mnaweza kurudisha uhai na soko lenu la filamu kama zama zile. Sitaki kuamini kama kweli alipofariki msanii mwenzenu Steven Kanumba basi kweli alikufa na tasnia nzima ya filamu. Lakini kwa muonekano huu inaonesha ni kweli Kanumba alipoaga dunia na sanaa nzima ikawa imeaga dunia.
-GPL
>
No comments: