HIKI NDICHO KINACHOUA WATANZANIA BARABARANI

NI asubuhi saa 11:30 alfajiri eneo la Msata mkoani Pwani, wananchi wamejaa barabarani na kuziba njia. Wanazuia magari yanayotoka mikoani kwenda Dar es Salaam yasipite kadhalika, yanayotoka Dar yamezuiliwa pia mpaka kieleweke. Kisa ni nini? Wanakijiji wanalia kukithiri ajali kila siku watu wanagongwa. Jumapili ibada hazimaliziki bila kuuawa ama kujeruhiwa waumini watokao kanisani sababu ni mwendo kasi wa madereva wasiojali vivuko vya wanaotembea, mikusanyiko, sehemu za ibada, shule, misikiti na hifadhi za taifa kuwa ni sehemu ya kupunguza mwendo. Madereva wanaua watu kwa ulevi, mwendokasi, magari mabovu, barabara mbovu na kubwa zaidi kuongozwa na sheria ya usalama barabarani iliyopitwa na wakati.

Ndiyo maana wadau mbalimbali wa usalama barabarani wanapendekeza marekebisho makubwa ya sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973, ambayo ina kasoro nyingi zinazoifanya kuwa chanzo cha ajali nchini. Miongoni mwa maeneo wanayoshauri yapitiwe upya ili kuboreshwa ni pamoja na matumizi ya mikanda. Sheria ya sasa ya usalama barabarani inasema ni kosa kisheria kwa dereva na abiria anayekaa kiti cha mbele kutokufunga mkanda wakati wa safari lakini haizungumzii lolote kwa abiria wanaokaa viti vya nyuma. Licha ya kanuni za Mamlaka ya Udhibiti wa Usafirishaji wa Ardhini na Majini (Sumatra) kumtaka abiria yeyote kufunga mkanda, kwa vile sheria mama (Road Traffic Act of 1973) ipo kimya katika eneo hilo utekelezaji wa kanuni hii unakwama.

Pia eneo jingine ni pamoja na matumizi sahihi ya kofia ngumu, kwa upande huu sheria ya sasa ya usalama barabarani inatambua kosa kwa mwendesha pikipiki kutokuvaa kofia ngumu lakini haisemi chochote kwa abiria anayepanda katika chombo hicho wala kutaja aina na ubora wa kofia inayofaa. Katika siku ya kuwakumbuka waliokufa ama kuumiziwa na ajali za barabarani iliyofanyika hivi karibuni ikiratibiwa na Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa) kwa kushirikiana na mtandao wa wadau kutoka asasi za kiraia unaotetea marekebisho ya sheria na sera za usalama barabarani umeiomba serikali kuifanyia maboresho sheria hii ya mwaka 1973 ili iweze kukabiliana ipasavyo na ajali za barabarani pamoja na athari zake.

Pamoja na mambo mengine, katika kuadhimisha siku hiyo tunaisihi serikali na watunga sheria kuifanyia maboresho Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 ili iweze kukabiliana ipasavyo na suala la ajali za barabarani pamoja na athari zinazotokana na ajali hizo,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa Edda Sanga. Aidha, anawasihi wananchi kuwa na tahadhari watumiapo vyombo vya moto bila kujali upungufu uliopo kwenye sheria za usalama barabarani ili kupunguza matukio ya ajali. “Mwendokasi umeendelea kuwa sababu kubwa ya ajali zinazoua watu wengi. Sheria yetu inao upungufu mfano kifungu cha 51(8) kinatambua maeneo machache katika kuzuia mwendokasi, ni muhimu.

               Sasa itamke maeneo yote na si yale ya mjini tu au makazi ya watu wengi. Iweke wazi kuhusu maeneo ya shule, nyumba za ibada, viwanja vya michezo na mbuga za wanyama,” anaongeza Sanga . Kwa matumizi ya vilevi na uendeshaji vyombo vya usafiri, sheria ya sasa ya usalama barabarani inasema kuwa itakuwa kosa kwa mtu yoyote kuendesha chombo cha moto akiwa na kiwango cha kilevi katika damu yake kinachozidi asilimia 0.08. “Kiwango hiki ni kikubwa sana kikilinganishwa na tafiti zilizofanywa na Shirika la Afya Duniani na kupendekeza kiwe asilimia 0.05 kwa dereva aliyebobea na asilimia 0.02 kwa dereva mchanga. Hivyo basi ni rai yetu sheria ifanyiwe marekebisho ili iendane na kiwango cha sasa cha kimataifa kilichofanyiwa utafiti,” anasisitiza Sanga.

Aidha, anaongeza kuwa adhabu zinazotolewa kwa sasa hazikidhi wala kuleta hofu kwa maderava wasiotaka kutii sheria na kanuni hivyo kuendelea kufifisha juhudi za kudhibiti tatizo la ajali za barabarani. Mwendokasi umeendelea kuwa sababu kubwa ya ajali zinazoangamiza watu wengi. Sheria inao upungufu hivyo kukwamisha udhibiti uendeshaji wa kasi kubwa miongoni mwa madereva. Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Pwani, Salumu Morimori, anasema wadau wa usalama barabarani wamekutana, kupokea na kutoa maoni yao juu ya mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya usalama barabarani sura ya 168. Anasema mapendekezo hayo yako katika mchakato ili kupelekwa bungeni kwa ajili ya marekebisho kwa baadhi ya vipengele baada ya wadau kutoa maoni yao na mapendekezo kuhusiana na sheria hiyo.

Mchakato wa marekebisho ya sheria hii ukikamilika, utasaidia kuwabana madereva wanaokikuka sheria za usalama barabarani. Awali haikuwa wazi kuhusiana na kufunga mkanda kwa abiria wa magari ya umma mabasi na haikuelekeza vizuizi vya watoto kwenye kiti cha gari lakini pia uvaaji wa kofia ngumu haukuelezwa kwa waendesha boda boda,” anasema. Mwenyekiti wa Usalama Barabarani Mkoa wa Pwani, anasema azma ya serikali na wadau wengine ni kuimarisha, kwa pamoja wanapambana na kila mmoja kwa nafasi yake kutimiza wajibu katika mapambano ya ajali za barabarani. “Shime kwa wadau kushirikiana na serikali kuhakikisha inaharakisha mchakato hudhibiti na kuwabana madereva wazembe na watumiaji wa barabara wanaokiuka sheria na kusababisha ajali. Tunataka Tanzania bila ajali na hili ni jambo linalowezekana.” Anasema Morimori.
>

No comments: