MAJANGA : MADAI YA KUSIKITISHA, BABA AZAA NA BINTIYE!

Dunia imekwisha! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kufuatia jamaa mmoja mkazi wa Mabibo-Mahakama ya Ndizi kudaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaye hadi kuzaa naye mtoto wa kike.
TUJIUNGE NA MAMA MZAZI
Akizungumza na gazeti hili kwa majonzi, mama mzazi wa binti huyo, Sakina, alidai kuwa alianza kusikia fununu juu ya uhusiano kati ya bintiye Mwanaisha na mumewe tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
“Nilisafiri kwenda Tanga, niliporudi ndipo nikaanza kusikia fununu kwa majirani kwamba mwanangu ana uhusiano na mume wangu,” alidai mama huyo.
Alidai alipojaribu kuhoji aliishia kupigwa mateke na mumewe huku akimwambia asisikilize maneno ya uongo kutoka kwa watu wenye chuki naye.
“Kiukweli moyo wangu uliniuma sana baada ya kupata taarifa hizi za mwanangu kutembea na mume wangu niliyezaa naye watoto sita.
“Roho iliniuma kama mzazi lakini pia kwetu huu ni mkosi mkubwa mno kwenye familia. Baada ya kufahamu niliamua kumhoji mtoto lakini hakuweza kunieleza lolote lile, nilipomhoji mume wangu yeye aliishia kunipiga mabuti tena mbele za watu,” alidai Sakina.

MAMA AZIDI KUFUNGUKA
Huku akifuta machozi, mzazi huyo aliendelea kusimulia kuwa, wakati huo tukio hilo linatokea, walikuwa wakiishi Kigogo Ruanga na baada ya suala hilo kuwa zito kwenye familia mumewe alimtimua pamoja na wanaye na akakimbilia maeneo ya Mabibo kujihifadhi kwa rafiki yake.
“Roho inaniuma sana, kwangu huu ni unyama wa kutisha na dira ya maisha yangu yote imeharibika. Mbali na hilo mwanaume huyu ameamua kunivua nguo na kunifedhehesha,” aliendelea kusimulia mama huyo.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
MWANAISHA ANASEMAJE?
Kwa upande wake Mwanaisha mwenye umri wa miaka 19, akizungumza na Amani namna alivyoanza kushiriki tendo la ndoa alisema hivi;
“Mimi baba alinibaka. Nakumbuka ilikuwa ni mwezi wa kwanza siku moja asubuhi baada ya mama kuondoka kwenda kwenye biashara zake aliingia chumbani na kisu.
“Alianza kunilazimisha kufanya naye mapenzi huku akinitishia kwamba endapo sitakubali kile anachokitaka basi atanichinja.
AMKUBALIA
“Nikakubali tukafanya mapenzi, lakini huo ndiyo ukawa utaratibu wake, kila mara mama alipokuwa hayupo nyumbani alinifuata akiwa na kisu mkononi na kunitishia tukafanya mapenzi mpaka nilipopata ujauzito,” alisimulia Mwanaisha.
Amani lilimuuliza Mwanaisha kama alitoa taarifa hizo za kubakwa na baba yake kwa mtu yeyote yule baada ya kufanyiwa kitendo hicho lakini alisema hakufanya hivyo kwa sababu aliogopa kuchinjwa kama ambavyo baba yake alikuwa akimtishia.
“Niliogopa kumwambia mtu yeyote yule baada ya baba kunitishia kuniua. Nikaamua kukaa kimya mpaka pale mama alipokuja kufahamu mwenyewe ukweli, naye aliumia sana,” alisema Mwanaisha.
Mwanaisha aliendelea kusimulia kuwa anajutia suala lililotokea kati yake na baba yake huyo wa kufikia ambaye ameanza kuishi naye tangu mwaka 2009, na kinachomfanya ajute zaidi ni kwa sababu mwanaye anamhesabu ni kama hana baba.
“Mwanangu ni kama hana baba. Huyo ni mume wa mama yangu sasa atakuwaje baba wa mtoto wangu pia.
“Kiukweli naumia na ikiwa Watanzania watanihurumia naomba wanisaidie maana ninaishi maisha mabovu sana mimi na familia yangu na hatuna hata uhakika wa kula ingawa nina kichanga,” alisema Mwanaisha.
MAMA MZAZI TENA…
Alipoulizwa Sakina kwamba mumewe huyo kwa sasa yupo wapi, alisema alikamatwa na polisi Jumamosi iliyopita baada ya kumripoti na mpaka gazeti hili linakwenda mitamboni, alikuwa akishikiliwa kwenye Kituo cha Polisi cha Urafiki.
“Yupo polisi Urafiki, anashikiliwa kwa kesi hii na Mungu akipenda tutampeleka mahakamani kwa kitendo alichokifanya ili iwe fundisho kwa kina baba wenye tabia kama zake na ninaomba hata waziri anayehusika na masuala ya jinsia (Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu) atusaidie,” alisema Sakina.
Amani lilifanya jitihada za kumtafuta Waziri Ummy lakini bahati mbaya halikufanikiwa kumpata.
KAMANDA AZUNGUMZA
Alipotafuta Kamanda wa Kinondoni, ACP Murilo Jumanne Murilo ili aweze kuzungumzia tukio hilo, alisema ndiyo kwanza analisikia na akaomba muda ili aweze kulifuatilia.
Kwa mtu yeyote atakayeguswa na maisha magumu anayoishi kwa sasa Sakina na mwanaye anaombwa kutoa msaada kwa namba; 0654527544.
Stori: Boniphace Ngumije na Ally Katalambula, Amani | DAR ES SALAAM
>

No comments: