MBUNGE GODBLESS LEMA AFUNGUKA KUHUSU RAIS MAGUFULI KUSAMEHE WAFUNGWA
Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema amempongeza Rais John Magufuli kwa kutoa msamaha kwa wafungwa.
Pia, amemshauri kuwaangalia mahabusu waliokaa muda mrefu gerezani pasipo kupata haki.
Katika maadhimisho ya uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara) jana Jumamosi Desemba 9,2017 mkoani Dodoma, Rais Magufuli alitoa msamaha kwa wafungwa 8,157 kati yao 1,828 waliachiwa huru kuanzia jana.
Rais John Magufuli leo Jumapili Desemba 10,2017 ametia saini nyaraka za msamaha alioutoa kwa wafungwa 61 waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa na wawili Nguza Viking na Johnson Nguza (Papii Kocha) waliohukumiwa kifungo cha maisha jela.
Akizungumza na MCL Digital, Lema amesema kuna mateso wanayopata mahabusu ambayo yanahitaji kuangaliwa.
“Rais Magufuli, Mungu akubariki kwa msamaha uliotoa jana kwa wafungwa na hasa wale waliokaa magereza muda mrefu pamoja na wazee, msamaha ni ibada,” amesema Lema ambaye pia ni mbunge wa Arusha Mjini (Chadema).
“Ni msamaha muhimu kwao, mtu aliyehukumiwa maisha au kifo akipata msamaha ni jambo jema sana, ninafurahi wamesamehewa sasa hawatakuwa tena magereza maisha yao yote,” amesema.
Lema amesema, “Nimefurahi kwamba hata wale waliokuwa wamehukumiwa kunyongwa hasa wazee pia wamepata msamaha, kwangu ninaona ni jambo jema na zuri, kwa mtu anayejua huzuni ya magereza atakubaliana nami.”
Kuhusu mahabusu, Lema amesema, ‘’Wako mahabusu wamekuwa magereza kwa muda mrefu bila kesi zao kukamilika. Mheshimiwa Rais fuatilia watu kama hawa pia.”
Na Ibrahim Yamola, Mwananchi
>
No comments: