Mtwara: Mwanamke Amfungia Mumewe Ndani na Kisha Kumchoma Moto
Jeshi la Polisi Mkoani Mtwara linamsaka mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Zuhura Ismail (29) kwa tuhuma za kumuua mume wake baada ya kumfungia ndani na kisha kuichoma nyumba kwa petroli.
Taarifa hizo zimetolewa na Kamanda wa Polisi mkoani humo Lucas Mkondya, ambapo amesema kwamba chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi, baada ya mwanamke huyo kugundua kuwa aliyekuwa mume wake anaishi na mke mwingine, na kuamua kumvizia nyumbani kwake kisha kuichoma moto na kusababisha kifo chake.
"Ni kweli Jeshi la Polisi Mkoani Mtwara linamsaka mwanamke mmoja ayefahamika kwa jina la Zuhura Ismail kwa tuhuma za kuichoma nyumba aliyokuwa anaishi mume wake na mwanamke mwingine, kutokana na wivu wa kimapenzi baada ya Zuhura kugundua kuwa mumewe anaishi na mke mwingine, na kuamua kwenda kuchoma nyumba hiyo moto na kuwasababishia majeraha makubwa, ambapo mumewe alipelekwa hospitali lakini kutokana na majereha hayo makubwa alifariki dunia, lakini mwanamke aliyekuwa nae anaendelea vizuri", amesema Kamanda Mkondya.
Aidha Kamanda Mkondya amesema mara baada ya tukio hilo mwanamke huyo aliyefahamika kwa jina la Zuhura Ismail alitoroka na kwenda kusikojulikana, na Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka na pindi atakapopatikana watatoa taarifa.
>
No comments: