Majengo Ya Wizara ya Maji Yaanza Kubomolewa Kutekeleza Agizo la Rais Magufuli

TINGATINGA limeanza kubomoa majengo ya Wizara ya Maji yaliyopo eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam kufuatia amri ya Rais John Magufuli aliyoitoa hivi karibuni.

Jengo lingine ambalo lkinatarajia kubomolewa na tingatinga ni la Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), ambalo linatazamana na wizara ya maji eneo la Ubungo.

Majengo hayo yanatakiwa kubomolewa ili kupisha ujenzi wa barabara itakayoanzia Ubungo hadi Chalinze mkoani Pwani kwa njia sita.

Leo asubuhi majengo hayo ya wizara yameanza ‘kupigwa nyundo’ ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli ambaye aliagiza majengo ya wizara hiyo na ghorofa la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuwekwa alama ya X kwa ajili ya kubomolewa.

Novemba 15,2017 akitokea Chato alipokwenda kwa mapumziko baada ya ziara ya Uganda, Rais Magufuli aliagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuweka alama ya X katika jengo la Tanesco na Wizara ya Maji, sehemu zilizo katika hifadhi ya barabara.

Katika majengo ya Wizara ya Maji, tingatinga limevunja ukuta, huku watu wengine wakiendelea na kazi ya kuondoa madirisha na milango kwenye majengo. Jengo lililoanza kubomolewa ni la ofisi ya Waziri wa Maji.

Wafanyakazi wa wizara hiyo wanaendelea kutoa mali ndani ya majengo waliyokuwa wakiyatumia kwa ofisi.

Mbali ya majengo hayo, Tanraods inaendelea kuweka alama ya X kwenye nyumba za wananchi zilizo katika hifadhi ya barabara ikiwa ni pamoja na kupisha ujenzi wa barabara za juu eneo la Ubungo.

Tayari nyumba takriban 1,200 zikiwamo tano za ibada, vituo vya mafuta na baa katika eneo la Ubungo hadi Kimara mwisho zimewekwa alama kwa ajili ya ubomoaji.

Kwa mujibu wa Tanroads, ubomoaji katika eneo la Ubungo hadi Kimara mwisho unahusisha nyumba zilizo mita 91.7 katika hifadhi ya barabara ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Hifadhi ya Barabara ya mwaka 1932.
>

No comments: