TRAFIKI ADAIWA KUFUMANIWA NA MKE WA MTU NDANI YA GARI

Fumanizi lenyewe.
Hili ni fumanizi la kufunga mwaka! Ndivyo walivyosikika wapenda ubuyu baada ya kushuhudia tukio la trafiki aliyefahamika kwa jina la Rajab kufumaniwa akiwa ndani ya gari na mke wa mtu aitwaye Marry.
NI MOROGORO
Tukio hilo lililojaza umati lilitokea Ijumaa iliyopita majira ya saa tatu usiku maeneo ya Forest mkoani Morogoro, jirani na nyumbani kwa mume wa Marry aitwaye Dunia.
NI TRAFIKI WA MSAMVU
Trafiki huyo anayedaiwa ni wa Kituo cha Polisi cha Msamvu kilichopo geti Kuu la Stendi ya Mabasi ya Msamvu, kitengo cha ukaguzi wa mabasi ambapo alikutwa amezima gari lake kwenye giza huku akiwa na Marry ambaye naye anafanya kazi ya kukusanya ushuru wa mabasi kwenye geti kuu la stendi hiyo ya Msamvu.
OFM ATONYWA
Sekunde chache tu baada ya kutokea kwa tukio hilo, rafiki mmoja wa mume wa Marry, alimtonya Kamanda wa kikosi cha Operesheni Fichua Maovu cha Global Publishers (OFM) ambaye alifika eneo la tukio na kushuhudia mtiti huo wa fumanizi ukiendelea huku mwenye mke akiwa na panga mkononi akitaka kumkata trafiki huyo anayedai kuiyumbisha ndoa yake.
Wakiwa kwenye gari usiku.
ASKARI WAMZUIA OFM
Katika hali ya kushangaza, baada ya Kamanda wa OFM kutinga eneo hilo la tukio na moja kwa moja kutimiza wajibu wake wa kupiga picha, askari waliokuwepo eneo hilo walimzuia asimpige picha mwenzao huku wakitishia kumnyang’anya kamera yake.
BODABODA WAMSAIDIA OFM
Hata hivyo, kamanda huyo alikomaa nao huku akipata sapoti kubwa kutoka kwa madereva wa bodaboda waliopambana kuhakikisha anapata picha.
RAIA KIBAO WATINGA
Ndani ya muda mfupi, wapenda ubuyu kibao walifika eneo hilo na kuanza kumtetea kamanda wa OFM ili aweze kutimiza majukumu yake ndipo askari hao walipolazimika kuwa wapole na kuamua kumzunguka Rajab aliyekuwa ndani ya difenda ili asipigwe picha.
Aibu yao.
WAMFUNIKA NA SHUKA
Ukiacha na askari hao kumzingira mgoni, baadhi yao walionekana wakimfunika na shuka la kimasai na kuondoka naye fasta eneo hilo huku gari la Rajab likiendeshwa na trafiki mwenzake akiwa na Marry ndani ya gari hilo.
UTETEZI WA RAJAB
Awali, Rajab, baada ya kumuona kamanda wa OFM alijitetea kwa kusema: “(akitaja jina la mwandishi wetu) hapa hakuna fumanizi huyu dada nimempa lifti tu, nimefika hapa, mumewe anadai amenifumania.”
MARRY ANASEMAJE?
Kesho yake, gazeti hili lilimpigia simu Marry na alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo alisema: “Mimi na mume wangu tumejenga huku Forest eneo la Wamo juu ya Milima ya Uluguru. Kila siku ninarudi nyumbani kwa bodaboda. Jana usiku Rajab alinipa lifti na tukiwa njiani alisimamisha gari ghafla na kumuona mume wangu akiwa na mwanangu mkubwa akidai amenifumania.
“Yeye (mumewe) mwenyewe anajua mimi ninaumwa, nina uvimbe tumboni na ninajiandaa kufanyiwa operesheni kwa hiyo ninaomba achana na habari hiyo.”
Mashuhuda wa tukio hilo.
MUME AFUNGUKA
Kwa upande wake Dunia alipohojiwa kuhusu tukio hilo, alikuwa na haya ya kusema: “Kazi yangu ni fundi wa magari kwenye Gereji ya Simba Oil. Mara nyingi nimekuwa mtu wa kusafiri sana, nikiwa safarini huwa ninaambiwa mke wangu niliyezaa naye watoto wawili, huwa ananisaliti na Trafiki Rajab ambaye yuko naye pale Stendi ya Msamvu.
“Wapambe wangu waliniambia kila siku mke wangu akitoka kazini, anapanda gari la Rajab. Siku ya tukio, mchana niliamua kupeleka malalamiko yangu kwa Mkuu wa Trafiki wa Wilaya, nikiomba Rajab ahamishwe eneo lile ili kulinda ndoa yangu na maelezo yangu yapo pale kituoni.
“Cha ajabu usiku wa siku hiyohiyo, jamaa zangu waliniambia mke wangu anapanda tena gari la Rajab, nikamwambia bodaboda awafuatilie kwa nyuma hadi wanapoishia.”
“Walipofika maeneo haya ya Forest wakasimamisha gari, wakafunga vioo. Kama unavyojua mimi na mke wangu tumejaliwa kupata watoto wawili na tumejenga huku Forest eneo la Wamo hivyo nilimchukua mwanangu mkubwa nikashuka naye na kumkuta mke wangu akiwa ndani ya gari na Rajab.
“Walikuwa wameloki milango. Baada ya kuniona, fasta Rajab aliwapigia simu askari wenzake, wakaja na kuanza kuzuia watu wasipige picha ukiwemo wewe (mwandishi wa Ijumaa Wikienda).”
Katika hali ya kushangaza, wakati tunakwenda mitamboni, Dunia alipiga simu kwenye gazeti hili akiomba habari hiyo isiruke hewani na uchunguzi wa awali uliofanywa na mwandishi wetu ulionesha kwamba Dunia ametishwa na Rajab kwamba habari hiyo ikitoka atamshitaki kwa kumtishia panga.
Kwa mujibu wa Dunia, kwa sasa kesi hiyo iko kwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro.
Ijumaa Wikienda lilifika ofisini kwa Kaimu Kamanda huyo na kuambiwa yupo nje ya ofisi hivyo gazeti hili linaendelea kufuatilia sakata hilo kujua mwisho wake.
STORI: DUNSTAN SHEKIDELE, IJUMAA WIKIENDA | MOROGORO
>

No comments: