Simba SC yaleta beki Kisiki Mghana






Beki huyo alitua juzi Jumamosi kwa ajili ya mazungumzo na Wekundu hao jambo linaloashiria kuna staa mmoja wa kigeni atakwenda na maji siku si nyingi.
Habari za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema mchezaji huyo mwenye kimo kama cha Juuko Murshid, ana nafasi kubwa ya kusajiliwa kwenye dirisha dogo kuchukua nafasi ya Laudit Mavugo anayekwenda Gor Mahia ya Kenya kwa mkopo.
Ujio wa mchezaji huyo aliyefikia hotelini Kariakoo, unamaanisha Joseph Omog lazima afanye maamuzi magumu kama bado ana msimamo wa kumsajili straika wa Rayon ya Rwanda, Shazir Nahimana.
POSHO JUU
Kama ulikuwa haujui mashabiki wa Simba kila mechi huwa wanachanga Sh5 milioni huku bilionea, Mohammed Dewji ‘MO’ naye akitoa Sh5 milioni na kuwakabidhi wachezaji endapo tu watashinda mchezo huo.
Hadi sasa msimu huu, Simba imeshinda mechi sita hivyo imetumia kiasi cha Sh60 milioni kwa ajili ya posho. Mkwanja huo hukabidhiwa kwa nahodha wa timu, Method Mwanjali, mara tu mechi inapomalizika naye hugawa kwa wachezaji wenzake kwa kadiri walivyokubaliana.
Mgawanyo ulivyo
Kwa wale wanaoanza pamoja na walioingia mchezoni baadaye hupata Sh400,000 kila mmoja, waliokaa benchi lakini hawakucheza kila mmoja anapewa Sh300,000 na waliokaa jukwaani hupata Sh150,000 ikiwa ni shukrani kwa kufanya mazoezi na wenzao.
Mmoja wa wachezaji wa Simba, alisema: “Huwa naumia ninapokosa nafasi ya kucheza maana kiwango huathirika na posho nayo hushuka pia.”
TRA WANENA
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo, alisema; “Tunafahamu Simba wanatoa pesa hiyo na wanaingizie serikali pato lake. Kila wanapofikia mwisho wa mwaka huwa tunaangalia kiasi gani wametumia na walichoingiza basi hapo na makato yetu hufanyika.”
TIMU NYINGINE
Wakati Simba na Yanga zikiwa na utamaduni wa kugawa pesa papo kwa papo kila baada ya mechi kumalizika, timu nyingine zimekuwa na utamaduni tofauti.
Azam wao wanatoa posho kwa wachezaji wao, lakini huwa wanawapa mwisho wa mwezi kwa kuongeza katika mishahara yao.
Mtibwa na Kagera Sugar nao wana utamaduni kama wa Azam ambao mishahara na posho ya aina yoyote ile lazima itolewe mwisho wa mwezi kipindi ambacho mchezaji analipwa chake kutokana na jasho alilotoa.
>

No comments: