Zitto Kabwe Apigilia Msumari Mapambano Dhidi ya Rushwa
Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe amesema licha ya Serikali kuonyesha juhudi za kukabiliana na rushwa, jitihada hizo hazitakuwa endelevu endapo taasisi za uwajibikaji hazitaachwa zifanye kazi kwa uhuru na uwazi.
Akizungumza katika mjadala ulioandaliwa na taasisi ya Twaweza leo Jumatano Novemba 29,2017, Zitto amesema taasisi kama Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG); Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA); kamati za Bunge za hesabu na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) zinapaswa kuachwa huru ili zifanye kazi kwa ufanisi.
Mjadala huo umelenga kuangalia ni namna gani ufa uliopo kati ya nia ya Serikali ya kupambana na rushwa kwa uwazi dhidi ya utamaduni wa usiri na porojo za kisiasa zinazoonekana kushamiri serikalini.
Zitto amesema kuendelea kuingiliwa kwa taasisi hizo kunasababisha mambo kufanyika ndivyo sivyo.
Ametoa mfano wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Chato akisema haieleweki mradi huo umeendeshwaje.
"Hatukatai Chato kuwa na uwanja wa ndege kwa sababu ni sehemu ya Tanzania; kinachoibua maswali ni namna mradi ulivyotekelezwa,” amesema.
Zitto amesema, "Hakukuwa na bajeti, zabuni hazikuwekwa wazi; aliyeshinda haijulikani ameshindaje na tunasikia hajawahi kujenga uwanja wowote."
Amesema taasisi za Serikali ikiwemo ofisi ya CAG na PPRA zilitakiwa zitoe taarifa ya kina kuhusu ujenzi huo.
Akizungumza katika mjadala huo, mwanzilishi wa mtandao wa JamiiForums, Maxence Mello amesema kuna haja ya Serikali kuongeza uwazi katika uendeshaji wa shughuli zake.
"Kuendelea kuweka mambo siri kunawafanya watu waibue vitu vingine ambavyo vingezuilika endapo wangekuwa wanafahamu kinachoendelea," amesema.
Mello amesema, "Kuficha mambo haisaidii na itasababisha Serikali iliyopo ikiondoka madarakani nyingine itakayochukua hatamu itaibua mambo ya ajabu."
>
No comments: