Breaking News: Aliyekamatwa na bilioni 2 Airport afikishwa mahakaman

Siku chache baada ya Rais John Magufuli kubainisha kukamatwa kwa kiasi kikubwa cha fedha katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA) aliyekamatwa na fedha hizo amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mshtakiwa huyo ni Raia wa Uganda, ambaye ni Kalani wa Kampuni ya Ulinzi ya SGA, Winfred  Businge  (33).

Busige amefikishwa mahakamani akikabiliwa na kosa la kushindwa kuelezea kwa mamlaka ya forodha fedha alizokamatwa nazo Airpot ambazo ni USD Milioni moja(takribani Sh.Bil 2).

Wakili wa serikali Mwandamizi, Awamu Mbagwa amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa mshtakiwa anakabiliwa na kosa moja.

Amedai kuwa kosa hilo amelitenda kinyume na kanuni za sheria za utakatishaji fedha, ambayo haimnyimi mshtakiwa dhamana.

Wakili Mbagwa amedai kuwa Businge ametenda kosa hilo December 11, 2017 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Inadaiwa akiwa ndani ya jiji la Dar es Salaam alikutwa ameingia nchini akiwa na USD Milioni 1 (zaidi ya Sh.Bil 2) ambazo alishindwa kuzitolea maelezo kwa wakala wa forodha.

Baada ya kusomewa kosa hilo, mshtakiwa alikana kosa, ambapo wakili Mbagwa alieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na anaomba tarehe kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali.

Hata hivyo, wakili wa utetezi Emmanuel Safari alimuombea dhamana mteja wake.

Hakimu Shaidi alimuachia mshtakiwa huyo kwa masharti ya dhamana ya mdhamini mmoja bila kusaini bondi.

Hakimu Shaidi amesema amemuachia kwa dhamana bila bondi kwa sababu fedha zilizokamatwa zitakuwa kama dhamana yake. Kesi imeahirishwa hadi January 18,2018.
>

No comments: