CCM yapewa meno dhidi ya Serikali

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli ametoa onyo kwa viongozi wa Serikali na hasa anaowateua kuwaheshimu na kuzingatia maagizo yanayotolewa na viongozi wa chama hicho, vinginevyo atawachukulia hatua.

Dk Magufuli aliitoa kauli hiyo jana mara mbili alipokuwa anafungua mkutano mkuu wa chama hicho asubuhi na akairudia tena alipokuwa anaufunga usiku.

Katika mkutano huo uliofanyika siku nzima na kuonyeshwa muda wote moja kwa moja na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC1), Magufuli alichaguliwa na wajumbe wa mkutano huo kuwa mwenyekiti wa CCM kwa kipindi cha miaka mitano baada ya kupigiwa kura zote 1,828 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete.

“Viongozi wa Serikali wanapaswa kutambua kwamba viongozi wa CCM ndio hasa wanaostahili. Kiongozi wa Serikali wa cheo chochote anawajibika kwa viongozi wa CCM,” alisema Rais Magufuli na kuamsha shangwe kutoka kwa wajumbe wa mkutano huo.

“Viongozi wa Serikali katika ngazi yoyote watambue kuwa waajiri wetu wakuu ni CCM, mimi bila CCM nisingekuwa Rais, CCM ndiyo kimejadili jina langu. Tupo hapa kwa ajili ya kutekeleza ilani ya CCM na wenye ilani hiyo ni hawa hapa (wajumbe) nendeni mkawasikilize,” alisema.

Dk Magufuli alionya asijitokeze kiongozi yeyote wa Serikali wa kusema hayajui (mambo) ya CCM.

“Kama mimi Rais niliyewateua ninayajua ya CCM asitokee mtu yoyote akasema hayajui mambo ya chama changu,” alisema.

Hata hivyo, alisema kauli hiyo isiwavimbishe kichwa viongozi wa CCM na kufanya mambo kinyume wakitegemea uongozi wao ndani ya chama hicho tawala.

“Nataka viongozi wa CCM kuheshimu viongozi wa Serikali na viongozi wa Serikali kuheshimu sana sana sana viongozi wa chama,” alisisitiza.

Katika mkutano huo, Magufuli alichaguliwa kwa kupata kura zote 1,828, huku makamu mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula akichaguliwa kwa kura 1,827. Makamu mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein akichaguliwa kwa kura 1,819.

Viongozi hao watatu walichaguliwa kwa kupata asilimia 100 ya kura zilizopigwa.

Mkutano huo pia uliwachagua wajumbe 30 wa Halmashauri Kuu (NEC) kati yao 15 kutoka Tanzania Bara na 15 wa Zanzibar.
>

No comments: