Chadema Singida, Wamgeuka Mbowe, Wasimamisha Mgombea

Wakati zikiwa zimebaki siku 25 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo katika  Jimbo la Singida Kaskazini, kivuli cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Lazaro Nyalandu kimeigawa Chadema katika pande mbili.

Wakati Chadema taifa kikiwa kimeeleza kutoshiriki katika uchaguzi huo Januari 13 mwakani kwa madai ya kutokuridhishwa na uchaguzi wa udiwani wa Kata 43 uliofanyika Novemba 26, uongozi wa Chadema mkoa wa Singida jana umempitisha mgombea atakayepeperusha bendera ya chama hicho.

Uchaguzi wa jimbo hilo unafanyika baada ya Nyalandu kutangaza kujivua uanachama wa CCM Oktoba 30 na kujiunga na Chadema huku mrithi wake akikigawa Chama chake kipya cha Chadema.

Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Singida, Shaban Limu amesema leo Desemba 19  kuwa  wamemteua Djumbe David Joseph kupeperusha bendera ya Chadema na msimamizi wa uchaguzi wilaya ya Singida naye amempitisha.

“Leo tunatarajia kufanya kikao cha kuweka mikakati ya kampeni. Kesho na kesho kutwa, tutaingia kazini kwa kufanya kampeni zitakazokileta chama matokeo tunayoyatarajia ambayo ni kushinda uchanguzi huo mdogo,” alisema Limu

Mbali na Djumbe, wagombea wengine na vyama vyao kwenye mabano ni Dalphina Patrice Mlewa (CUF), Omari Mohammed Sombi (Alliance for Tanzania Farmers Party), Monko Justein Joseph (CCM), Aloyce Mohammed Nduguta (Ada Tadea) na Mchungaji Samwel Libisu (CCK).

Wagombea hao walitangaza jana Desemba 18, 2017 na Msimamizi wa uchaguzi wilaya ya Singida, Rashid Mandoa amesema wamepitisha wagombea hao baada ya kukidhi vigezo vyote vinavyo hitajika.

Mandoa amesema wagombea kutoka vyama vya NRC na UMD wao hawakupitishwa baada ya kushindwa kukidhi vigezo. Pia wagombea kutoka UDP na UDPP hawakurudisha fomu.

Akizungumzia uamuzi huo, Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema; ‘’kwa mjibu wa Katiba ya Chadema, Kamati Kuu ndiyo inayopitisha jina la mgombea na Kamati Kuu haijakutana sasa hilo jina limepatikanaje.”

“Tutashangaa hata NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) kama wataendeleza mchakato wa jina hilo na tumeagiza tuletewe taarifa na hatua zitachukuliwa kwa wahusika kwani kilichofanyika ni kosa la jinai, kama barua ya Katibu Mkuu kuthibitisha kupitishwa na Chama haipo wao wameitoa wapi,” amehoji Mrema

Amesema kama kuna watu wametumiwa basi watambue kwamba msimamo wa chama haujabadilika na wanafuatilia suala hilo na hatua zitachukuliwa kwa viongozi waliohusika.
>

No comments: