Rose Muhando Atangaza Kujiunga na Chama cha Mapinduzi CCM

Msanii wa nyimbo za Injili aliyetamba kwa vibao vyake murua na vyenye kuburudisha Rose Muhando, ametangaza kujunga rasmi na Chama cha Mapinduzi.

Msanii huyo ambaye aliomba kujiunga na chama hicho amekabidhiwa kadi ya Chama cha Mapinduzi leo yeye pamoja na kikundi chake, katika Mkutano Mkuu Maalum wa Tisa wa CCM Taifa, unaofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, mjini Dodoma.

Rose Muhando kabla ya kukabidhiwa kadi ya chama cha CCM alitumbuiza kwa kibao maalumu alichokiandaa kwa ajili ya Rais John Pombe Magufuli ambacho amekipa jina la “Magufuli Tubebe”.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey polepole alitangaza kuwa Rose Muhando pamoja na Kundi lake wameomba kupewa nafasi ya kutumbuiza kwa wimbo huo maalumu pamoja na kukabidhiwa kadi za CCM.

“Kundi la Ndugu Rose Muhando na yeye mwenyewe niwakaribishe Jukwani kwa wimbo ambao wameutunga maalumu kwa Ndugu Magufuli. Kundi hili walipokuwa wanakuja walikuwa na maombi mawili, ombi la kwanza ni kupewa nafasi ya kuimba wimbo huu maalumu na pili kujiunga rasmi na CCM,” amesema katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole.

Hata hivyo Polepole amesema kuwa Rose Muhando na kundi lake watakabidhiwa kwa makatibu wa mikoa husika kwa ajili ya michakato ya kuwaandikisha kama wanachama wapya wa CCM.
>

No comments: